Sunday, January 4, 2015



Hii ni picha ya mashelisheli mabichi.Mashelisheli ni chakula adhimu kwa waswahili. Mashelisheli huchumwa kutoka juu ya mshelisheli. Huwezi kuyala mashelisheli kabla ya kuyapika. Waswahili wanakula mashelisheli wakati wa chai ya asubuhi, wakati wa chakula cha mchana na wakati wa chakula cha usiku.

Baada ya kuchumwa, mashelisheli humenywa na kukatwa mapande.


Haya ni mapishi tofauti ya mashelisheli na namna linavyoliwa kwa vitooyo tofauti. Njia rahisi ya kula shesheli ni kulikata mapande na kulichemsha. Baada ya kuchemshwa watu hupenda kula shelisheli kwa dagaa, samaki wa kukaanga au wa kuchemsha na pia huliwa kwa mboga hasa ya ntoriro.Kama watu hawamiliki kitooyo, hula shelisheli la kuchemsha  tupu au kwa achari.
Kama ukiwa na nazi basi shelisheli la nazi ni tamu maradufu. Baada ya kumenywa shelisheli hukatwa vipande vidogo vidogo. Shelisheli la nazi linaweza kuliwa kwa nyama ya ng'ombe kwa samaki au hata kuchanganywa na dakaa kavu.
Pia shelisheli huliwa na kitafunwa baada ya kukaangwa. Baada ya kulimenya unalikata vipande vyembamba kwa kulikaanga kwenye mafuta. Baada ya kulitoa kwenye mafuta unalinyunyizia chumvi. Baada ya hapo huwa liko tayari kuliwa kwa kachumbari ya tungule na vitunguu iliyokolea ndimu na pilipili hoho na kuchanganywa na duvi.
Pia kuna watu wanapenda ponde ya shelisheli. Hili ni shelisheli ambalo huchemshwa na baadae kuchanganywa na tui na nazi(machicha ambayo hayajakamuliwa). Mchanganyiko huu hutiwa na ndani ya kinu na kutwangwa na baadae  huwa tayari kuliwa hasa kwa mchuzi wowote wa nazi au dikodiko la pweza mvunza.

No comments: